Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Sayyid Bahauddin Naqshbandi, kiongozi wa twariqa ya Naqshbandiyya huko Kurdistan ya Iran na Iraq, katika warsha ya tano ya kimataifa isemayo: "IranJukwaa la Heshima ya Kiislamu katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni" iliyoandaliwa kwa juhudi za Majma‘u-l-‘Ālamī Qādimūn, aliutambulisha utawala wa Kizayuni kuwa ni adui wa pamoja wa Uislamu na ubinadamu, na akasisitiza juu ya ulazima wa mshikamano wa Umma wa Kiislamu.
Sheikh Sayyid Bahauddin Naqshbandi, akirejea hali ya kibinadamu nchini Palestina, alisema: Mauaji ya watoto, wanawake na raia wasio na hatia huko Ghaza yanaonesha kuwa kinachoendelea ni jinai iliyoratibiwa na ya wazi dhidi ya ubinadamu.
Akiweka wazi kuwa utawala wa Kizayuni tangu mwanzo wa kuundwa kwake umejengwa juu ya dhulma na uvamizi, aliongeza: Utawala huu daima umejitahidi kudhoofisha Umma wa Kiislamu kwa kuchochea migawanyiko ya kimadhehebu, kikabila na kisiasa, na kile tunachokishuhudia leo ni muendelezo wa sera hiyo ya kihistoria ya kupinga heshima na umoja wa Waislamu.
Kiongozi wa twariqa ya Naqshbandiyya alisema kupinga Uzayuni kuwa ni wajibu wa kidini, kimaadili na kibinadamu, na akasisitiza: Kusimama dhidi ya uvamizi si msimamo wa kisiasa pekee, bali ni jukumu la kisheria ambalo Qur’ani Tukufu, mwenendo wa Mtume Mtukufu (s.a.w.) na Mawalii wa Mwenyezi Mungu wamelisisitiza, na kila Mwislamu huru anapaswa, kwa kadiri ya uwezo wake, kuchukua msimamo dhidi ya dhulma hii iliyo wazi.
Akitoa shukrani kwa misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuwaunga mkono wananchi wa Palestina, alisema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, licha ya mashinikizo, vikwazo na vitisho vya mara kwa mara, imesimama bega kwa bega na watu madhulumu wa Palestina, na msimamo huu wa kishujaa unastahili pongezi na heshima.
Sheikh Naqshbandi, akisisitiza umuhimu wa umoja wa Waislamu, alibainisha: Heshima ya Uislamu iko katika mshikamano na umoja wa Umma wa Kiislamu, na maadamu Waislamu watabaki katika mifarakano, maadui wa Uislamu wataendelea kutumia mianya hii vibaya. Leo, zaidi kuliko wakati mwingine wowote, kuna haja ya kuungana katika kauli moja na ushirikiano kati ya mataifa na serikali za Kiislamu.
Kiongozi wa twariqa ya Naqshbandiyya, katika hitimisho, alieleza matumaini yake kwamba, kwa kuamka Umma wa Kiislamu na kuimarika kwa mhimili wa muqawama, jinai dhidi ya watu wa Palestina zitakoma, na akasema: Kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu na kwa umoja wa Waislamu, siku ya kuikomboa Palestina na kumalizika dhulma na uvamizi iko karibu.
Maoni yako